Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, shirika hilo limetoa wito huo baada ya Dkt. al-Singace kukaa gerezani kwa miaka 16 na kuendelea na mgomo wake wa chakula kwa kipindi cha miaka mitano, kufuatia kunyang’anywa maandishi yake ya utafiti.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti yake, shirika hilo lilieleza kuwa limetuma barua kadhaa kwa mtawala wa Bahrain, Hamad Isa Al Khalifa, pamoja na Mwanamfalme na Waziri Mkuu wake, Salman Hamad Al Khalifa, likitaka hatua zichukuliwe kuhusu suala la Dkt. al-Singace.
Dkt. al-Singace, ambaye anatumikia kifungo cha maisha nchini Bahrain, alikamatwa baada ya kushiriki katika maandamano ya kuunga mkono demokrasia yaliyofanyika Machi 2011, na kudai haki zake katika maeneo ya uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani—haki ambazo zote zinatambuliwa na kulindwa chini ya Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa.
Shirika hilo lilieleza kuwa Dkt. al-Singace alianza mgomo wake wa chakula tarehe 8 Julai 2021, akipinga hatua ya mamlaka za gereza kunyang’anya maandishi yake ya utafiti kuhusu lahaja za Bahrain za lugha ya Kiarabu. Maandishi hayo, kwa mujibu wa taarifa hiyo, alikuwa ametumia miaka minne kuyatafiti na kuyaandika.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, chakula chake kimekuwa kikitegemea virutubisho vya vitamini vya majimaji pekee. Aidha, bado anashikiliwa katika Kituo cha Huduma za Afya cha Al Muharraq, huku akisumbuliwa na matatizo mbalimbali ya kiafya, akinyimwa fursa ya kupata dawa, na pia kuzuiwa kupata magazeti pamoja na vituo vya televisheni vya kidini.
Shirika hilo lilisisitiza kuwa taarifa zinazoeleza kuzorota kwa hali ya afya ya Dkt. al-Singace na mahitaji yake ya haraka ya matibabu, pamoja na kuwekwa kwake kizuizini kwa muda mrefu na kuhukumiwa bila ushahidi wa kutosha, zinaonyesha kupuuziwa kwa kiwango cha kutia wasiwasi kwa viwango vya kimataifa vinavyohusu taratibu stahiki za kisheria, kesi ya haki na kizuizi cha mtu.
Shirika hilo limeeleza kuwa, viwango hivyo vimehakikishwa katika Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa, ambao Bahrain pia ni mwanachama wake.
Hatimaye, shirika hilo limewataka viongozi wa Bahrain kuhakikisha usalama na afya ya Dkt. al-Singace akiwa kizuizini, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha anatembelewa mara kwa mara na familia yake, huduma endelevu za matibabu, pamoja na kumwachilia huru.
Aidha, limetaka kuondolewa mashtaka au hukumu yoyote inayohusiana na utekelezaji wa amani wa haki zake za kibinadamu.
Maoni yako